Kampuni inayojishughulisha na kilimo cha Mpunga ijulikanayo kwa jina la Highland Estates iliyopo wilayani Mbarali Mkoani Mbeya imepewa mwezi mmoja kuhakikikisha inasafisha mifereji yote inayozunguka shamba lao kwa kujenga upya miundombinu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Richard Muyungi amesema kuwa viongozi wa shamba hilo wafanye juhudi za ziada kutunza mazingira yote yanayowazunguka ili kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi katika mifereji ya matoleo ya kupeleka maji Mto Ruaha Mkuu.
“Tunawapa mwezi mmoja mfanye ukarabati na mrekebishe hali ya usafi katika mifereji ya shamba lenu baada ya muda huo tutarudi kwa ajili ya kukagua.” Amesema Muyungi
Aidha, Kikosi kazi hicho pia kilitembelea katika shamba jingine la Mwekezaji lililopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya lijulikanalo kwa jina la Kapunga Rice Project na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wakulima katika bonde hilo.
Hata hivyo, Kikosi kazi hicho cha Kitaifa kilichopo Mkoani Mbeya bado kinaendelea na ziara ya kutembelea sehemu mbalimbali ili kiweze kupata maoni ya Wananchi kuhusu kitu kinachozuia maji kuingia Mto Ruaha.