Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa wenye matatizo kama Magonjwa, Wazee, Wajawazito, Walioingia na watoto, Walemavu, na wenye matatizo ya akili.
Aidha, msamaha huo ameutoa katika Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliyofanyika mapema hii leo mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira imesema kuwa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anayo Mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa
Ameongeza kuwa msamaha huo hautawahusu wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha na wale waliofungwa kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya, waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, na wale wenye makosa ya kujihusisha na utoaji na uombaji rushwa.
Wafungwa wengine ambao hawatahusika na msamaha huo ni pamoja na wale wanaotumikia kifungo cha makosa ya shambulio la Aibu, Kunajisi, Ubakaji, Kulawiti, Utekaji, Utumiaji vibaya madaraka.
Hata hivyo, Wafungwa 2,219 watafaidika na msamaha huo na wataachiliwa huru na kurejea uraiani kushirikiana na jamii katika ujenzi wa Taifa na kujiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena Gerezani.