Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Serikali itaboresha maslahi na mazingira ya wafanyakazi nchini na kuleta maendeleo.
Ameyasema hayo mapema hii leo alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi duniani iliyofanyika Kitaifa Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Amesema kuwa Serikali inajali maslahi ya wafanyakazi na inashughulikia madai yao na kusema kuwa kila kitu kitakuwa sawa ikiwa ni pamoja na kupandishiwa mshahara.
“Tumeamua kusafisha nyumba iliyokuwa imejaa uchafu, hawa viongozi wa TUCTA wanastahili sifa kwa sababu wanafanya kazi ya kutetea maslahi ya wafanyakazi,”amesema Rais Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa mwaka huu Serikali ina mpango wa kuajiri wafanyakazi hamsini elfu ambapo itasaidia kuongeza ufanisi Serikalini.
Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Serikali ina nia thabiti ya kujenga nchi na si kuendekeza masuala ya ujanja ujanja.