Kikosi cha Mbeya City leo kitaanza safari ya kurejea jijini Mbeya, baada ya kumaliza kambi ya mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, ambayo ilikua na lengo la kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Young Africans.
Kikosi cha Mbeya City kiliweka kambi mjini humo, ikiwa ni sehemu ya mapendekezo yaliyotolewa na uongozi wa benchi la ufundi chini ya kocha kutoka Malawi, Kinnah Phiri.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu ya Mbeya City Dismas Ten, ameiambia Dar24 kuwa, dhumuni kubwa la kuweka kambi mjini Sumbawanga lilikua ni kufanya maandalizi, ambayo yataendana na hali ya hewa ya jiji la Dar es salaam, ambapo watakapocheza dhidi ya Young Africans Mei 14.
Amesema waliona kuna haja ya kuweka kambi mjini Sumbawanga, kutokana na ukaribu uliopo pamoja na uhakika walioupata wa kucheza michezo ya kirafiki dhidi ya timu za mkoani Rukwa.
“Tunaamini maamuzi yetu ya kwenda Sumbawanga yalikua sahihi na tumefanikiwa kucheza michezo minne ya kirafiki ambayo itatusaidizi kufanya vizuri katika mchezo wetu dhidi ya Young Africans.”
“Tunajua mchezo utakua mgumu na ndio maana kocha wetu ameamua kuutumia vizuri muda huu wa mapumziko ya ligi, ili kupata kambi ya muda mrefu sambamba na kucheza michezo ya kirafiki.”
“Tunarejea Mbeya leo na tutafanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza safari ya kuelekea jijini Dar es salaam, kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Young Africans Mei 14.” Amesema Dismas.
Mbeya City ilikabliwa na matokeo mabovu katika michezo minne waliyochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Kumbukumbu Ya Sokoine Jijini Mbeya, hali ambayo ilizua taharuki kwa mashabiki wao na kufikia hatua ya kuutaka uongozi wa juu kuwatimua wahusika wa benchi la ufundi.
Mbeya City walitoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya African Lyon na Ruvu Shooting, kabla ya kupoteza dhidi ya Ndanda FC kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.