Rais wa Marekani, Donald Trump amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Urusi, Vladimir Putin kuhusu njia ya kumaliza mgogoro wa Korea Kaskazini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa leo na Ikulu ya Marekani, wakuu hao wa nchi walifanya mazungumzo jana jioni ikiwa ni mara ya tatu kufanya mazungumzo kwa njia hiyo.
Imeelezwa kuwa kati ya mambo yaliyozungumziwa ni pamoja na namna ya kuweza kutatua mgogoro wa majaribio ya makombora ya kinyuklia yanayofanywa na Korea Kaskazini, ikiwa ni wakati ambao nchi hiyo imeendelea kusisitiza utekelezaji na mpango wake wa majaribio ya makombora hayo licha.
Marekani imesogeza meli zake kadhaa za kivita karibu na rasi ya Korea kwa lengo la kujipanga kuikabili Korea Kaskazini endapo itaendelea kukaidi makatazo ya kutoendelea na majaribio hiyo. Hata hivyo, Korea Kaskazini imeonya kuwa itaingia kwenye vita kamili endapo itashambuliwa kwa namna yoyote ile.
Katika hatua nyingine, marais hao wa mataifa makubwa na yenye nguvu duniani walizungumzia namna ya kuweza kusitisha mashambulizi nchini Syria. Mwezi uliopita Marekani ilishusha makombora mazito kama adhabu ya tuhuma za kuwepo kwa shambulizi la mabomu ya kemikali yaliyodaiwa kufanywa na Syria ambayo ni mshirika wa Urusi.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema kuwa mbali na hayo, walijadili na kukubaliana kushirikiana dhidi ya makundi ya kigaidi katika nchi mbalimbali pamoja na matendo yanayofanywa kinyume na haki za binadamu.
Tangu alipokuwa akiwania nafasi ya Urais wa Marekani, Trump alionesha msimamo wa kuwa na urafiki na Urusi ambayo ilikuwa ikichukuliwa kama hasimu wa Marekani katika nyanja mbalimbali katika kipindi cha mtangulizi wake, Barack Obama.