Klabu ya Simba imesema inasubiri kupewa barua na Shirikisho la soka nchini (TFF) inayoonyesha kweli wamepokwa pointi tatu za mchezo dhidi ya Kagera Sugar ili wakashtaki kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo CAS.
Simba SC ambayo ilipoteza mchezo huo mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, ilikabodhiwa pointi tatu baada kamati ya usimamizi na uendeshwaji wa ligi (Kamati ya saa 72) kujiridhisha kuwa, Kagera walimchezesha beki Mohamed Fakih ambaye alikuwa na kadi tatu za njano kabla ya mchezo huo, pointi ambazo baadae zilirejeshwa kwa Kagera na kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, Rais wa klabu hiyo Evans Aveva amesema hawawezi kukubali kuona timu yao inaonewa tena na TFF, na kwa kuanzia wanasubiri wapewe barua ya kupokwa pointi tatu ili wapeleke malalamiko yao CAS.
“Tumeonewa mara nyingi, mfano suala la wachezaji Mbaraka Yusuph, Hassan Kessy na Ramadhan Singano ‘Messi’ walikuwa wachezaji wetu halali lakini TFF wakawaidhinisha kucheza timu nyingine, huu ni uonevu tumechoka kuonewa tunaenda FIFA,” alisema Aveva.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56 na michezo miwili mkononi ambayo ikishinda yote itaizidi Simba kwa pointi tatu.