Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uandishi katika kuandika habari zitakazoleta umoja, mshikamano na maendeleo na siyo uchochezi ili kujenga jamii bora.
Hayo yamesemwa mapema hii leo Jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani na Mbunge wa viti maalumu wa CUF mkoa wa Dar es salaam, Salma Mwasa.
Amesema kuwa Tasnia ya habari inatakiwa kuheshimiwa kama zilivyo zingine hivyo chama cha wananchi CUF kiko tayari kushirikiana na wanahabari kutetea maslahi yao.
“Chama cha Wananchi CUF kinaungana na waandishi wa habari kusherekea maadhimisho haya ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kwani tunatambua umuhimu wa waandishi na changamoto mnazokumbana nazo, hivyo tuna ahidi kuwa nanyi bega kwa bega,“amesema Mwasa.
Hata hivyo, ameongeza kuwa pamoja na kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, kalamu ya mwandishi wa habari ni lazima itetee ukweli wa jambo na si vinginevyo.