Mshambuliaji kinda wa vinara wa ligi ya nchini England (Chelsea) Betrand Traore, ameiwezesha klabu ya Ajax Amsterdam anayoitumikia kwa mkopo, kupata ushindi katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Europa League dhidi ya Olympic Lyon ya Ufaransa.
Traore alifunga mabao mawili kati ya manne yaliyoiweka Ajax Amsterdam katika mazingira mazuri ya kutinga kwenye hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Hata hivyo Olympic Lyon walipata bao la kufutia machozi na kuufanya mchezo huo uliochezwa Amsterdam Arena kumalizika huku ubao wa magoli ukisomeka 4-1.
Traore ambaye ni raia wa Burkina Faso amefunga mabao hayo katika dakika za 25 na 71. Mabao mengine ya Ajax yakifungwa na Kasper Dolberg katika dakika ya 34 na Amin Younes katika dakika ya 49 na bao la Lyon limefungwa na Mathew Valbuena katika dakika ya 66.
Huo ni ushindi wa 12 mfululizo kwa Ajax nyumbani katika michezo 12 iliyopita ya michuano mbalimbali.
Michuano hiyo itaendelea tena hii leo kwa mchezo wa pili wa nusu fainali ambapo Man Utd watakua ugenini wakicheza dhidi ya Celta Vigo nchini Hispania.