Baada ya kupigiwa kura za hapana kwa wagombea wa ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ezekiah Wenje na Lawrence Masha katika uchaguzi uliopita majina yao kwa mara nyingine yamejumuishwa na mengine manne ili kukamilisha watu sita watakao chuana kugombania nafasi hizo.
Hyo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika alipokuwa akizungumza na kituo kimoja cha televisheni mjini Dodoma.
Amesema kuwa wameamua kuyarudisha majina hayo mawili ili kuleta Demokrasia ya kweli katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani wagombea hao ndio walikuwa chaguo la chama hicho.
“Tumeamua kuyarudisha tena majina ya wagombea hao ili tuweze kuitendea haki Demokrasia ya nchi yetu, tunaamini kuwa majina haya yataleta changamoto kubwa kwenye bunge la Afrika Mashariki kamaya yatapitishwa,”amesema Mnyika.
Hata hivyo, majina ya wagombea wengine walioteuliwa ni pamoja na Prof. Abdallah Safari, Salum Mwalimu, Josephine Leymon na Pamela Massy.