Mlinda mlango wa Young Africans Beno Kakolanya, amesema haoni tatizo kuwekwa benchi na kocha George Lwandamina, ambaye ana malmlaka ya mwisho ya kupanga kikosi cha kwanza.
Kakolanya alijiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea Tanzania Prisons ya jijini Mbeya, ambapo amekuwa akipigania namba dhidi ya Deogratius Munishi “Dida” na Ally Mustafa “Barthez” ambao hutumika mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.
“Tangu mwanzo watu walikuwa wanasema siwezi kupata namba Yanga lakini wanasahau kuwa mpaka hivi sasa nimeshacheza mechi nne kwenye kikosi cha kwanza na nimefanya vizuri,” Alisema kipa huyo.
“Kucheza mechi nne kikosi cha kwanza mbele ya wazoefu wawili sio jambo dogo, hasa kwa nafasi zetu za makipa ambazo hazifanyiwi mabadiliko ya mara kwa mara,”
“Kocha yupo sahihi na nianamini kadri siku zinavyokwenda nitapewa mechi zaidi na kupata uzoefu mkubwa, nafanya mazoezi, siamini kama naweza kushuka kiwango.” Aliongeza.
Klabu ya Yanga iliamua kumsajili kipa huyo ili kuongeza ushindani kwenye nafasi ya mlinda mlango ambayo kwa muda mrefu ilitawaliwa na makipa wawili ambao ni Dida na Barthez.