Halmashauri zote nchini zimeagizwa kuhakikisha zinajenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya hasa maeneo ya vijijini ili kuweza kuwaweka karibu wakunga ambao wamekuwa wakitoa huduma ya dharura kwa akina mama wajawazito na watoto.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani.

Amesema kuwa Halmashauri zikijenga nyumba karibu na vituo vya kutolewa huduma za afya zitasaidia kupunguza matatizo ya mama na watoto wanaotaka kupata huduma za dharura.

Aidha, Samia suluhu amesema kuwa changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini Serikali inaendelea kuzifanyia kazi ikiwemo uboreshaji wa maslahi kwa watumishi wa kada hiyo pamoja na kuongeza maradufu vifaa tiba. .

Makamu wa Rais pia amewahimiza wakunga kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia maadili na waache tabia ya kutoa lugha mbaya kwa wanawake wajawazito na wakunga watakaobainika kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali ili kukomesha tabia hiyo.

Hata hivyo, Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia ipasavyo utoaji bora huduma za afya kwa wananchi pamoja na kusimamia maadili kwa watumishi wa sekta ya afya kote nchini.

 

Majaliwa anunua hisa Vodacom, awasihi wananchi wanunue kabla muda haujaisha
Beno Kakolanya: Ninaheshimu Maamuzi Ya Lwandamina