Bingwa wa dunia wa uzito wa ‘welterweight’ mwenye mkanda wa Shrikisho la Masumbwi Duniani (WBO), Manny Pacquiao amemualika tena bondia Floyd Mayweather kupanda ulingoni akidai kuwa hajawahi kufikiria kama alishindwa pambano lao la kwanza.
Pacquiao ambaye anajiandaa na pambano lake dhidi ya bondia wa Australia, Jeff Horn, ameviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa angependa sana kukutana tena na Mayweather ulingoni kwakuwa hivi sasa ameshapona kabisa majeraha ya bega.
“Ningependa kufanya pambano la marudiano na Mayweather kwa sababu hivi sasa bega langu limepona kabisa,” alisema Pacquiao. “Lakini pambano la marudiano linategemeana na yeye kama anataka kupigana tena,” aliongeza.
“Sijawahi kufikiria kwamba nilipoteza lile pambano [dhidi ya Mayweather],” alisisitiza.
Pacquiao alipoteza kwa Mayweather mwaka 2015, katika pambano lililoweka rekodi kubwa duniani kimapato na msisimko, likipewa jina la ‘Pambano la Karne’.
Baada ya pambano hilo, Pacquiao alidai kuwa alikuwa na tatizo la bega aliloumia katika mazoezi. Madaktari walifanikiwa kumfanyia upasuaji baadae kabla hajarudi tena ulingoni thidi ya Timothy Brandley na kuibuka mshindi.
Bondia huyo wa Ufilipino aliyestaafu na kurejea tena ulingoni, pambano lake lililopita alishinda dhidi ya Jesse Vergas, na kuwa bondia wa kwanza kuwa na cheo cha Useneta huku akiwa bingwa wa masubwi duniani.
Pacquaio anatarajia kupanda jukwaani kutetea mkanda wake wa ubingwa, dhidi ya Jeff Horn wa Australia, pambano litakalofanyika nchini humo July mwaka huu.
Kwa upande wa Mayweather, alitangaza kustaafu masumbwi na amekuwa akiepuka kuzungumzia pambano la marudiano kati yake na Manny Pacquiao huku akisisitiza kuwa hata akipigana naye mara elfu moja, atamshinda kila pambano.