Mshambuliaji kutoka  nchini Senegal, Sadio Mane usiku wa kuamkia leo Jumatano, aliibuka kidedea kwa kutangazwa mshindi mara mbili wa kinyang’anyiro cha kumsaka mchezaji bora wa mwaka wa Liverpool msimu wa 2016/17 katika hafla ilizofanyika Anfield.

Mane ambaye kwa sasa anauguza jeraha la goti, alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa klabu na mchezaji bora wa mwaka chaguo la mashabiki, akimshinda mshindi wa mwaka jana wa tuzo hiyo Mbrazil, Philippe Coutinho.

Mane ameshinda tuzo hizo baada ya kuwa katika kiwango bora tangu alipotua Liverpool mwezi Agosti mwaka jana akitokea Southampton kwa ada ya Pauni Milioni 32.

Mpaka sasa Mane ndiye mfungaji bora Liverpool akiwa amefunga mabao 13.

Wengine waliochomoka na tuzo ni Trent Alexander-Arnold,18, aliyeshinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi. Ben Woodburn ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa kituo cha kulea na kukuza vipaji kwa vijana cha Liverpool (Academy).

Emre Can ametwaa tuzo ya bao bora la mwaka, baada ya bao lake la tiki taka alilofunga dhidi ya Watford juma lililopita kuonekana kuwa bora zaidi kuliko mabao yote yaliyofungwa na Liverpool msimu wa 2016/17.

Lucas Leiva amepewa tuzo ya heshima baada ya kufikisha miaka kumi (10) akiwa klabuni Liverpool. Tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa upande wa wanawake imeenda kwa Sophie Ingle.

UVCCM yang'aka, yawaonya wasaliti ndani ya jumuiya
Juventus FC Watangulia Millennium Stadium