Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Exim inatarajia kujenga nyumba 9500 za askari magereza ili kukabiliana na changamoto za makazi ya askari wa jeshi hilo hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akizungumzia changamoto za Makazi ya askari wa Jeshi la Magereza Nchini, katika uzinduzi wa Gereza la Wanawake wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Naibu Waziri Masauni amesema kuwa Serikali inatambua changamoto za makazi kwa askari magereza na tayari iko katika mazungumzo na benki ya Exim ili iweze kujenga nyumba hizo.

“Nawaomba askari wetu nchi nzima wawe na subira Serikali inatambua na inashughulikia changamoto ya makazi ya askari na tayari tuko katika mazungumzo na wadau ikiwemo benki ya Exim kuanza mradi wa ujenzi wa nyumba takribani 9500, lengo ni kukidhi kiu ya makazi ya askari na familia zao,” amesema Masauni.

Akitoa maelezo ya ujenzi wa Gereza hilo, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, Dk. Juma Malewa amesema kuwa ujenzi wa Gereza hilo umefanywa na wataalamu ambao ni askari Magereza kwa kushirikiana na wafungwa kama sehemu ya utekelezaji wa amri ya Mh. Rais Dk. John Magufuli ya kutaka wafungwa watumike katika kazi za uzalishaji ikiwemo kilimo, ujenzi na ufundi mbalimbali.

Kamishna Malewa amesema ujenzi wa Gereza hilo umegharimu jumla ya shilingi milioni 65 na litasaidia pia kuhifadhi wafungwa 148 na hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa katika Gereza la Kongwa mkoani Dodoma pamoja na kuepuka usumbufu wa ndugu wa wafungwa kusafiri mpaka wilayani Kongwa kwenda kuwaona ndugu zao.

?LIVE IKULU: Hotuba ya Rais Dkt. Magufuli na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini Ikulu Dar es salaam
Mbeya City FC yatamba kushusha kipigo dhidi ya Yanga