Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinatarajiwa kuburuzwa kortini na kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Alphonce Lusako anayedai kukatishwa  masomo yake kwa kufutiwa usajili wake januari 26 mwaka huu kwa madai ya kukiukwa kwa utaratibu wa usajili wake.

Alphonce aliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya kukishtaki chuo hicho kwa kumkatisha masomo yake ambapo amesema imemuathiri pakubwa kwani mpaka sasa hana kazi ya kufanya na anahisi ndoto zake zimezimwa na chuo hicho.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Florens Luoga amesema kuwa suala la kijana huyo analifahamu vizuri na kuongeza kuwa kila mwananchi ana haki ya kwenda mahakamani kudai haki yake anayohisi kaonewa.

“Hakuna anaezuiwa kwenda mahakamani kudai haki yake, mwache aende, tutaenda kujitetea huko kama ameonewa atapata haki yake na kama hajaonewa chombo cha sheria kitaamua, uamuzi wake wa kwenda mahakamani ni mzuri kwani anahisi kaonewa.,”amesema Prof. Luoga.

Prof. Luoga amesema kuwa wakati wa usajili chuo kilifuata taratibu zote ikiwa ni kipengele kwa kipengele na waliokuwa na sifa ya kuendelea na masomo chuoni hapo waliendelea na masomo na wale ambao hawakuwa na sifa waliweza kusimamishwa akiwemo Alphons.

Mwandishi Mahiri wa Habari za Dawa za Kulevya auawa kwa Risasi
Rais Magufuli aridhia ombi la kuacha kazi waliokuwa majaji, Mkuu wa Mkoa