Klabu ya Simba imewasilisha rasmi malalamiko yake FIFA kuhusu pointi tatu walizonyang’anywa na Shirikisho la Mpira wa Tanzania, TFF baada ya Kagera Sugar kumtumia mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Klabu hiyo, Geofrey Nyange Kaburu alipokuwa akizungumza na Clouds FM, amesema kuwa wanachosubiri kwa sasa ni kusikia ni uamuzi utatolewa na shirikisho hilo.
“Tumeshatuma malalamiko yetu na yamepokelewa FIFA, tumeainisha tunataka nini. Nisiwasemee, wao watasoma na wataamua halafu watatujulisha walichokiamua,” amesema Kaburu.
Hata hivyo, Simba wamefikia uamuzi wa kupeleka malalamiko yao FIFA baada ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za wachezaji kutengua uamuzi wa Kamati ya saa 72 ambayo awali iliipa Simba pointi tatu na magoli matatu baada ya kubaini ni kweli Kagera Sugar ilimchezesha Fakhi dhidi ya Simba huku akiwa na kadi tatu za njano kinyume na kanuni.