Mtoto Shukuru Kisonga mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Tunduru ambaye ameishi kwa kunywa mafuta ya kula lita moja, maziwa lita mbili na sukari robo tatu kwa siku amefanyiwa vipimo mbalimbali vya damu na kupata matibabu na sasa afya yake imeanza kuimarika.
Hayo yamebainishwa na Daktari, Stella Rwezaura ambaye anamtibu mtoto Shukuru, mara baada ya kukutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kuelezea juu ya ugonjwa unaomsumbua mtoto huyo ambapo ameeleza kua baada ya kumfanyia uchunguzi wamebaini anasumbuliwa na Selimundu (sickle cell).
Dkt. Rwezaura amesema kuwa kwa sasa mtoto Shukuru ameacha kutumia mafuta ya kula na Sukari na kuanza kutumia uji. Bofya hapa kutazama video
Hospitali ya Taifa Muhimbili ilichukua jukumu la kumtafuta na kumfanyia vipimo ili aweze kupatiwa matibabu mtoto huyo baada ya kupata taarifa zake kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ikionesha namna ambavyo akiteseka.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Mkuu wa kitengo hicho amasema kwa sasa mtoto huyo ataruhusiwa baada ya afya yake kuimarika na kwamba sasa hanywi tena vitu hivyo na hajabadilika rangi wala mwili kumuuma hali ambayo ilikua ikimsumbua.
Siku chache zilizopita Shukuru ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dar es salaam kwa ajili ya matibabu kutokana na tatizo hilo.