Rais wa Marekani, Donald Trump amekutana kwa mara ya kwanza na kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis katika mji wa Vatican.

Kwa mujibu wa CNN, wawili hao wamekutana kwa ajili ya maongezi ya faragha, huku baadhi ya wachambuzi wakidai kuwa suala la mvutano wa mpango wa Trump kujenga ukuta katika mpaka wa nchi yake na Mexico litajadiliwa.

Papa Francis alipinga wazi mpango wa Trump kujenga ukuta huo, wakati wa harakati za kampeni ya uchaguzi wa urais wa Marekani.

Hata hivyo, mgogoro wa Mashariki ya Kati unaweza kuwa alama nzuri zaidi ya kuwakutanisha kimawazo hasa baada ya Trump kuahidi kufanya awezalo kusaidia kupatikana kwa amani kati ya Israel na Palestina.

Trump ameingia Vatican akiwa na mkewe Malania na binti yake Ivanka, pamoja na mkwe wake, Jared Kushner, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kutembelea mataifa mbalimbali.

Kiongozi huyo wa Marekani atakutana pia na rais wa Italia na waziri mkuu wa nchi hiyo, kabla hajaelelkea Brussels kwa ajili ya kushiriki mkutano wa NATO.

Ugaidi: Polisi wauawa kwa Bomu la kutegwa ardhini
Waziri Dkt. Mwakyembe kuongoza mapokezi ya Serengeti Boys