Jeshi la polisi nchini Kenya limepata pigo la kigaidi alfajiri ya leo baada ya maafisa wake wanne kufariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa vibaya kwa bomu lililotegwa ardhini eneo la Liboi Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Tukio hilo la kigaidi limetokea katika eneo hilo karibu na mpaka wa nchi hiyo na Somalia, baada ya gari lililokuwa limewabeba askari hao kwa ajili ya doria kukanyaga bomu la kutegwa ardhini.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, maafisa hao walikuwa wanasafiri kwa gari la kituo cha polisi cha Kulan wakipitia barabara ya Liboi-Milan, kabla ya kukanyaga bomu hilo.
Serikali ya Kenya imelaani vikali tukio hilo la kigaidi. Kupitia akaunti yake ya Twitter, Makamu wa Rais wa nchi hiyo, William Ruto ameandika, “waathiriwa wa shambulio la Liboi kaunti ya Garissa wamo mawazoni mwangu. Ni lazima tuujenge ukuta mpakani.”
Kenya iliridhia kuwa itajenga ukuta kati ya nchi hiyo na Somalia, tangu mwaka 2015.
Nchi hiyo imekuwa ikipambana na magaidi wa kundi la Al-Shabaab ambalo limekuwa likitekeleza matukio ya kigaidi nchini humo. Mwaka 2015, magaidi hao walitekeleza shambulio kali katika chuo kikuu cha Garissa.
Jeshi la Kenya liko nchini Somalia likiendelea kuwashughulikia wanamgambo wa Al-Shabaab. Hata hivyo, hakuna kundi lililojitokeza hadharani kudai kutekeleza tukio hilo.