Taarifa za kukamatwa kwa njiwa aliyekuwa akisafirisha kete 178 za dawa za kulevya nchini Kuwait zimemuibua aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Mzowa kulizungumzia.
Mzowa ameeleza kuwa mtandao wa wafanyabishara wa dawa za kulevya ni mpana na kwamba hufanya vikao kubaini mbinu mpya kila kukicha kwa lengo la kukwepa nguvu za dola na kuingiza bidhaa hiyo haramu kwenye mipaka ya nchi zote.
“Wauza dawa za kulevya duniani wanafahamiana, wanawasiliana na wanafanya mikutano yao ili kuweka mikakati katika biashara zao. Wana uwezo wa kujua njia ipi ni salama kwa wakati fulani na katika nchi gani na wanakatiza mipaka ya mataifa yote,” Mzowa anakaririwa na Mwananchi.
“Ukitaka kujua uwezo wa wafanyabiashara hao haramu utakuta cocaine inatengenezwa Brazil lakini inakatiza mipaka yote mpaka inafika China. Kila siku wanabuni mbinu mpya, bila ushirikiano na nchi nyingine wataingia tu,” aliongeza.
Aidha, alieleza kuwa wakati alipokuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, kuna wakati wafanyabiashara hao walitumia boti zinazosafiri chini ya maji lakini walipobainika walianza kutumia mashua ambazo hutia nanga sehemu yoyote yenye ukingo wa bahari.
Mbinu ya kutumia njiwa kusafirisha dawa za kulevya iliwahi pia kubainika nchini Colombia mwaka 2011 na jijini Costa Rica mwaka 2015.
Dunia imebadilika, njiwa hatumiki kama ishara ya mjumbe mwema bali hadi kwenye uhalifu.