Dayow Mohamed Hassan mwenye umri wa miaka 44, amepigwa mawe hadi kufa kwa kosa la kufanya mapenzi nje ya ndoa.
Hassan ambaye ni raia wa Somalia, amekutwa na hukumu hiyo iliyotekelezwa na wanajeshi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab, katika eneo wanalolidhibiti.
Kwa mujibu wa BBC, adhabu hiyo ilitolewa kwa mujibu wa sheria kali baada ya kukutwa na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamke asiye mke wake na kumpa ujauzito, ingawa alikuwa na wanawake wawili wa ndoa.
Kesi hiyo iliyosikilizwa mahakamani kwa mujibu wa sharia ilifunguliwa na mwanamke aliyemlalamikia Hassan kwa kumbaka na kumpa ujauzito.
Gavana mtiifu kwa Al Shabaab, Moalim Geedow amesema kuwa mamia ya wananchi walikusanyika kushuhudia adhabu hiyo ya kupigwa mawe hadi kufa iliyotolewa katika kijiji cha Ramo Adey.
Mwaka 2014, kijana mdogo alipigwa mawe hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanamke mmoja. Pia, mwaka 2008 msichana mmoja alikubwa na hukumu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kufanya uzinzi.