Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ametoa taarifa mpya kuhusu hali ya watoto wanaopata matibabu nchini Marekani, baada ya kupata ajali wakiwa ndani ya basi la shule wilayani Karatu mkoani Arusha, ajali iliyochukua uhai wa wanafunzi zaidi ya 30.
Nyalandu ameeleza kupitia Twitter na Instagram kuwa watoto hao wanaendelea vizuri na kwamba Sadia Awadh na Wilson Tarimo wameanza kufanya mazoezi ya viungo.
“Sadia ameweza kuanza kusimama mwenyewe na anaendelea na MAZOEZI kama anavyoonekana pichani,” aliandika kwenye picha husika.
Jana jioni, alieleza kuwa watoto hao wawili walienda katika wodi ya watoto kwa lengo la kumtembelea mtoto mwenzao, Doreen Mshana kwenye wodi ya hospitali ya Mercy, jijini Sioux.
Watoto hao watatu, wahanga wa ajali ya basi la shule ya sekondari ya Lucky Vicent iliyotokea Mei 6 mwaka huu wilayani Arusha, walisafirishwa kwenda Marekani kwa ndege ya Shirika la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa Muhibiri maarufu duniani, Bill Graham.