Serikali imetanga kuongeza nguvu zaidi katika vita ya kupambana na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa ikiwa ni mkakati wa kutokomeza mtandao huo.
Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga ambapo amesema kuwa lengo kubwa la serikali ni kutokomeza mtandao mzima wa watu wanaojihusisha na biashara hiyo ili kuweza kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.
“Dawa za kulevya zinaathiri sana nguvu kazi ya Taifa na tangu Mamlaka hii imeanza tumefanikiwa kudhibiti uingizaji wa Heroine, Cocaine na dawa nyingine za kulevya na tumewakamata wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wanatafutwa na mataifa makubwa na hiyo ni hatua kubwa kwa nchi yetu katika mapambano haya,” Amesema Sianga. l
Hata hivyo, Sianga ameongeza kuwa Serikali imepanga kuongeza vituo vya kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya katika Mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mwanza kwa awamu ya kwanza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya na matumizi yake.