Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Morocco Herve Renard, amekiri kushtushwa na taarifa za mchezaji Hakim Ziyech aliyegoma kujiunga na wenzake kwenye kambi ya kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Cameroon Juni 10.
Herve Renard alitangaza kikosi cha Simba wa Atlas juma lililopita na alitarajia mchezaji huyo wa klabu za Ajax Amsterdam ya Uholanzi, angejiunga na wenzake juma hili lakini imekua tofauti.
Kocha huyo kutoka Ufaransa amewaambia waandishi wa habari kwamba, amesikitishwa na kitendo kilichoonyeshwa na kiungo huyo ambaye alipaswa kuwa mfano wa kuigwa.
Hata hivyo amesisitiza kwamba, kukosekana kwa Ziyech hakutomuharibia mipango yake kuelekea mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Uholanzi unaochezwa hii leo.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, aliwahi kuachwa na kocha Renard wakati wa kutaja kikosi cha mwisho kilichoshiriki fainali za Afrika za mwaka huu, ambazo ziliunguruma nchini Gabon.
Siku chache baadae kocha alimuita tena mchezaji huyo ili azibe nafasi ya Younes Belhanda aliyekua majeruhi, lakini alikataa kuitikia wito, jambo ambalo lilihisiwa huenda alichukizwa na kitendo cha kuachwa katika kikosi cha awali.