Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekana kipande cha sauti kilichosambazwa kwenye mitandao hivi karibuni kikidaiwa kuwa kilirekodiwa wakati wa maongozi kati yake na Wema Sepetu kwa njia ya simu, maongezi yanayosikika kuwa ya kimapenzi.
Akizungumza kupitia XXL ya Clouds Fm leo, Mbowe amesema kuwa sauti hizo zimetengenezwa kwa lengo la kumchafua na kwamba anaifananisha na taarifa za maji taka.
“Mimi ninalichukulia kama taarifa za kawaida ya maji taka ambazo zinasambazwa, taarifa ambazo zinatengenezwa hazina ukweli wala hazina msingi wowote ndo ambacho naweza kusema kwa sasa kwasababu hizo taarifa sio za kweli…timu yangu ya mtadao inajaribu kufatilia kujua zimeoriginate kwa nani” alisema Mbowe.
Mbunge huyo wa Hai ambaye ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alisema kuwa Wema ni mwanachama mpya wa Chadema na mtu maarufu anayemheshimu, na kwamba tangu azisikie sauti hizo kwenye mitandao hakuwahi kuzungumza naye kwakuwa hivi sasa wako katika shughuli za mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo.
Kwa upande wa Wema, aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram kuwa anaona kuna haja ya kubadili sauti yake kwa kuwa imekuwa rahisi kwa mtu huiigiza.
“There is a need to change my vocals maana zimekuwa too easy to imitate … this is just wrong… Heeeitooooz Y’all shud keep trying, u getting there… But I must say, Impressed,” Wema aliandika kwenye Instagram.