Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mary Shangali amewataka Mahakimu na wadau wa Mahakama nchini kote kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma ya haki kwa wananchi.
Jaji Shangali amesema hayo wakati alipokuwa akiongea na Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete pamoja na Gereza la Ludewa na Makete.
“Ushirikiano wa karibu na Wadau wa Mahakama kama Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawakili na Watumishi wa Mahakama n.k ni muhimu katika kutekeleza shughuli yetu ya utoaji haki kwa wananchi, jambo hili lina faida nyingi mojawapo ikiwa ni kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu,” alifafanua Mhe. Shangali ambaye pia ni Jaji namba moja (1) wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha, Jaji Shangali alibainisha changamoto alizokumbana nazo katika ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama mkoani Njombe kuwa ni tatizo kubwa la usafiri wa kuwachukua Mahabusu kutoka Magerezani na kuwarudisha.
Amesema kuwa changamoto hiyo haiihusu Mahakama moja kwa moja bali ipo chini ya Jeshi la Polisi, kwa kuwa Mahakama na Polisi wote wanafanya kazi kwa kutegemeana changamoto hiyo inaathiri na inaweza kusababisha mlundikano wa mashauri na Mahabusu magerezani kutokana na Wahusika wa kesi kutofikishwa Mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi zao kwa wakati stahiki.
Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo malalamiko mengine yaliyotolewa yaliwahusisha baadhi ya Mahakimu kuwa na tabia ya kutowasikiliza Washitakiwa kwa makini na hatimaye kutoa maamuzi tofauti na uhalisia wa shauri husika.
“Naomba niwaombe ninyi Mahakimu mliopo hapa na baadhi ya Mahakimu nchini kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa Weledi, kwani Mahakama ndio kimbilio la wananchi hivyo ni vyema kutoa nafasi kusikiliza kwa makini na usahihi pande zote ili kufanya maamuzi yanayostahili,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.
Aidha; Mhe. Jaji Shangali amesisitiza juu ya utoaji wa Adhabu Mbadala kwa watuhumiwa wenye makosa madogo madogo ili kuepuka mlundikano usio wa lazima magerezani.