Maisha ya mshambuliaji kutoka nchini Hispania Diego Costa ndani ya klabu ya Chelsea ni kama yamefikia tamati, baada ya meneja wa mabingwa hao wa England Antonio Conte, kupasulia ukweli kwa kumwambia hamuhitaji tena.
Costa amefichua siri ya ujumbe aliotumiwa na meneja huyo kutoka nchini Italia, kwa kusema Conte amemueleza hamuhitaji tena katika himaya yake, na amempa uhuru wa kuchagua pakwenda kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, alikua na mipango ya kutaka kuondoka Stamford Bridge mwanzoni mwa mwaka huu, kufuatia ofa aliyoipata kutoka Tianjin Quanjian ya mashariki ya mbali (China), lakini Conte aliweka mkazo wa kutomruhusu kuondoka.
Maamuzi ya Conte ya kumpa uhuru Costa kuondoka klabuni hapo, yamekuja kufuatia mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Everton, Romelu Lukaku, ambaye yu tayari kurejea Stamford Bridge.
Hata hivyo uongozi wa Everton umeshaeleza wazi thamani ya Lukaku kuwa ni pauni milioni 100, na Chelsea wanajipanga kusaka fedha za kujazia kitita cha kumsajili mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji.
Klabu ya ya zamani ya Costa, Atletico Madrid ipo tayari kumrejesha shujaa huyo, lakini wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kusajili hadi Januari 2018, iliyotolewa na shirikisho la soka duniani FIFA.