Klabu ya Manchester City imekamilisha dili la usajili wa mlinda mlango kutoka nchini Brazil na klabu ya SL Benfica ya Ureno Ederson Santana de Moraes, kwa ada ya Pauni milioni 35.
Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23, alikua kivutio kwa meneja wa Man City Pep Guardiola kutokana na kazi kubwa aliyoifanya msimu uliopita, ambapo aliisaidia SL Benfica kutwaa ubingwa wa Ureno.
Mkataba wa Ederson na Man City utaanza rasmi Julai Mosi mwaka huu, na ameahidiwa kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Guadiola ambacho msimu ujao kinatabiriwa kuwa na sura mpya.
Ederson, amesema anaamini ametua mahala salama, na anahusudu huduma ya ukufunzi inayotolewa na Pep Guardiola, hivyo atajifunza mambo mengi katika kipindi chote atakachokuwepo Etihad Stadium.
Juma lililopita uongozi wa SL Benfica ulitangaza kufikia makubaliano ya kumuuza mlinda mlango huyo, hatua ambayo ilidhihirisha nusu ya safari ya mlinda Ederson, ambaye alihitaji kusaka changamoto mpya ya soka lake.
Ederson aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Brazil chini ya umri wa miaka 23, na sasa ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha wakubwa ambacho kinaendelea kucheza michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunua za 2018. Mwishoni mwa juma hili Brazil itacheza dhidi ya Argentina na kisha Australia siku ya jumanne juma lijalo.
Ederson, anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa mlinda mlango mwingine wa Man City Claudio Bravo, ambaye mwanzoni mwa msimu uliopita alisajiliwa kutoka FC Barcelona, akichukua nafasi ya Joe Hart aliyepelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Torino ya Italia.