Klabu ya Olympic Lyon imeutaka uongozi wa Arsenal, kujiandaa kikamilifu endapo wanahitaji huduma ya mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Alexandre Lacazette.
Arsenal wanahusishwa na mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, na tayari meneja Arsene Wenger ameonekana mara kadhaa katika viunga vya ufaransa, na inadhaniwa anafuatilia mipango ya usajili wa wachezaji aliowalenga kutoka nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph, Olympic Lyon imewataka Arsenal iandae kitita cha Euro Milioni 55 (sawa na Pauni milioni 48.7) kama ada ya awali, kisha Euro milioni 12 (sawa na Pauni milioni 10.6) kama ada ya nyongeza kwa ajili ya mshambuliaji huyo.
Dai hilo limetolewa Rais wa Olympic Lyon, Jean-Michael Aulas ambaye mapema juma lililopita alikutana na meneja wa Arsenal Arsene Wenger pamoja na Mtendaji Mkuu, Ivan Gazidis.