Roma Mkatoliki amefunguka sababu za kuingia darasani na kufundisha somo la hisabati ikiwa ni miezi kadhaa ya ukimya wake kwenye muziki, tangu alipokumbwa na jinamizi la kutekwa na watu wasiojulikana.
Roma ambaye kitaaluma ni mwalimu aliyeingia kwenye tasnia ya muziki na kuendelea kuwafundisha watanzania kuhusu hali ya jamii na kisiasa inayoendelea, alisema kuwa aliamua kuingia shuleni hapo kama sehemu ya kurudisha shukurani kwa jamii kwa kile walichomfanyia.
Mkali huyo wa michano aliongeza kuwa alikuwa na lengo la kuwasilisha zawadi yake ya vitabu vya hisabati na kutoa neno kwa wanafunzi hao lakini sio kwamba ameamua kuacha muziki na kurejea darasani.
“Kilichotokea ni kwamba, ni kama nafanya ‘bring back to society’, kurudisha fadhira kwa jamii kutokana na tatizo ambalo limetokea na niliona jamii ilisimama na mimi sana. Jamii ni kubwa kuliko Roma, siwezi kufanya kila kitu, lakini ninaweza kufanya vitu vichache nikawagusa baadhi ya watu halafu wakawakilisha watu wengi,” Roma aliiambia Amplifaya ya Clouds Fm.
“Kwahiyo nikaona ndio wakati sahihi na jamii imesimama na mimi, basi ngoja nichague moja ya shule ambazo zina changamoto kubwa sana, kwahiyo ikaja tu nikachagua shule moja inaitwa Mchikichini shule ya msingi maeneo ya Mbagala. Nikaona niende kutembelea, na kubwa zaidi ni kuwapa neno ambalo litadumu kwenye vichwa vyao na kusikiliza kero zao, kwasababu mimi kama public figure ninaamini nina sauti ambayo ninaweza kuipaza watu wakatatua zile changamoto, aliongeza.
Alisema kuwa akiwa shuleni hapo aliamua kuingia na kukumbushia kufundisha somo la hisabati na kutoa zawadi yake ya vitabu vya somo hilo.
Katika hatua nyingine, kwa mara ya kwanza, Roma alionekana akiwa anamlinzi binafsi, kwa lugha ya kigeni Bodyguard katika tukio hilo. Huenda ni moja kati ya hatua za kujihami baada ya tukio lililomkuta yeye na wenzake wawili.