Serikali imesema kuwa haitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi nchini mpaka hapo hali itakapo kuwa shwari na kukomeshwa kwa vitendo hivyo.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani alipokuwa akifungua mkutano wa kimataifa wenye lengo la kubadilishana uzoefu katika kupambana na rushwa.
Amesema kuwa vita ya kupambana na vitendo vya rushwa ni kipaumbele cha kwanza katika Serikali ya awamu ya tano na wale wote wanaonufaika na kuwezesha vitendo hivyo wataendelea kuchukuliwa hatua.
“Kupambana na rushwa ni jambo la msingi na muhimu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu katika nchi yeyote Duniani,”amesema mama Samia Suluhu.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano ikiongozwa na Rais Dkt. Magufuli imejidhatiti na itaendelea kukaza kamba ili kuhakikisha inatokomeza vitendo vya rushwa ambavyo vinaonekana kukithiri.