Msanii mkongwe wa Hip Pop nchini, Afande Sele amemgeukia aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Jamal Malinzi na kuelezea hisia zake kuwa ni bora alivyofutiliwa mbali kwani katika uongozi wake hakuna jambo lolote la maendeleo alilolifanya.
“Ofisi ya chama cha soka cha Sudan na ofisi ya chama cha soka Tanzania..aibu yetu..acha Magufuli atunyooshe tu kwani tulizidisha uwendawazimu. Nenda Malinzi nenda tuuu” ameandika Afande Sele.
Afande Sele amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook na kuiponda Ofisi ya chama cha Soka Tanzania na Sudan na kuita aibu tupu, hivyo amesisitiza Magufuli aendelee kuwanyoosha.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Jamal Malinzi ambaye alikuwa ni mmoja kati ya watu ambao walikuwa wanagombea nafasi ya Urais katika shirikisho hilo lakini jina lake lilienguliwa katika mchakato huo baada ya kushindwa kuhudhuria katika usaili wa wagombea uliofanyika siku ambayo yeye yupo rumande kutokana na kesi inayomkabili ya matumizi mabaya ya ofisi.
Hata hivyo msanii huyo mkongwe wa Hip Pop aliyevuma sana na kibao chake cha Mimi ni msanii, ameamua kuupa kisogo mzuki huo wa hip pop na kuamua kujikita katika kukosoa mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.
Siku chache zilizopita Afande Sele alimponda msanii Vanessa Mdee na kusema halindi heshima ya muziki wa Tanzania kwani kwa anachokifanya yeye katika sanaa ni muziki wa kuiga toka mataifa ya magharibi.