Bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Pensheni wa PPF imepongezwa kwa uamuzi wa kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kujenga kiwanda kipya pamoja na kuendeleza kiwanda cha bidhaa za ngozi na Karanga Kilichopo Mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kutembelea na kuona maendeleo ya kiwanda hicho, ambapo amesema kuwa PPF na Jeshi la Magereza wamefanya maamuzi sahihi yanayoendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.
“Dhamira ya Serikali ni kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda, PPF na Jeshi la Magereza mmeonesha mfano, uboreshaji wa kiwanda hiki na ujenzi wa kiwanda kingine ambacho kitakuwa na viwanda vidogovidogo vinne ni ishara ya kutimia kwa ahadi ya Rais wetu Dkt. John Magufuli ya kuwa na uchumi wa kati kupitia Viwanda,”.amesema Mhagama.
Aidha, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha na Serikali itatoa msaada popote inapohitajika ili kwa haraka nchi yetu ianze kuzalisha viatu ambavyo vitauzwa nje ndani na nje ya nchi hatimaye kuliingizia taifa mapato.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa PPF na Jeshi la Magereza lazima wahakikishe mipango waliyoiweka ya ujenzi wa kiwanda kipya na maboresho ya kiwanda cha zamani yanafanyika kwa wakati ili kwa haraka uzalishaji uanze na hatimaye nchi iweze kunufaika.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameishauri mifuko mingine ya pesheni kutumia fursa zilizopo Jeshi la Magereza ikiwamo maeneo na rasilimali watu katika kufikia azama ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni za wastaafu PPF, William Erio amesema kuwa kiwanda hicho kitagharimu shilingi bilioni 54.4 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha na wanategemea kuzalisha futi mraba za ngozi Milioni tatu laki saba na nusu (3,750,000/=) kwa mwaka na kuongeza kuwa kiwanda hicho kitazalisha viatu vya kijeshi na kiraia jozi milioni moja na laki mbili kwa mwaka, pamoja na kutoa soli laki tisa kwa mwaka pamoja na kutoa bidhaa nyingine za ngozi kama mikanda,mabegi na mikoba