Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu jana alishikiliwa na jeshi la polisi kwa saa kadhaa wilayani humo akihusishwa na vurugu zilizoibuka ndani ya kikao cha ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Nagu ambaye alikuwa mmoja kati ya wajumbe wa kikao cha kamati ya siasa ya wilaya ya Hanang, alishikiliwa na jeshi la polisi baada ya kutokea mvutano mkali wa pande mbili zilizoibuka wakati wa mjadala wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Francis Masawe alithibitisha kukamatwa kwa Dk Nagu kutokana na vurugu hizo na kueleza kuwa aliandika maelezo na kuachiwa baada ya saa kadhaa.
“Taarifa ambazo nimezipata ameachiwa baada ya kuandika maelezo na tayari walifikia makubaliano wenyewe [pande mbili zilizosigana],” Kamanda Masawe anakaririwa na Mwananchi.
Dk. Nagu aliwahi kuwa waziri wa viwanda na biashara, pamoja na waziri wa katiba na sheria kwa nyakati tofauti katika awamu mbili za serikali zilizopita.