Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anadaiwa kugoma kupima mkojo kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alipopelekwa na Jeshi la Polisi.

Lissu ambaye alikamatwa na Jeshi la Polisi mwishoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa tuhuma za uchochezi, ameendelea kushikiliwa na jeshi hilo baada ya juhudi za mawakili wake kumtafutia dhamana kugonga mwamba.

Mke wa mbunge huyo wa Singida Mashariki, Alice aliwaambia waandishi wa habari kuwa mumewe alimwambia kuwa aligoma kupima mkojo kwa sababu kosa aliloshtakiwa nalo halina uhusiano na zoezi la kupima mkojo. Pia, alisema kuwa kuna taratibu za kufuatwa kabla ya kufanyiwa vipimo hivyo.

Taarifa hizo pia zimethibitishwa na mwanasheria wake, Peter Kibatala ambaye ameongeza kuwa Lissu amekataa kutoa maelezo yoyote polisi mpaka atakapofikishwa mahakamani.

Mke wa Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya zoezi hilo kushindikana, polisi walingozana na Lissu hadi nyumbani kwake ambapo walifanya upekuaji wa kina na kuondoka na baadhi ya vifaa vya kielekroniki kama CD na iPad.

Mwanasheria wa Lissu, Fatma Karume aliwaambia waandishi wa habari kuwa mteja wake hakupewa dhamana kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi na jeshi la polisi na kwamba wameamua kufungua shauri Mahakama Kuu kuiomba iamuru mteja wake apewe afikishwe mahakamani.

“Leo hii tumepeleka zile documents(nyaraka) ambazo mmeniona nasaini, ni documents za kuiomba mahakama iliambie jeshi la polisi limlete Tundu Lissu mahakamani Jumatatu, ili kama wana kesi waendelee na kesi na wamkabidhi Tundu kwa mahakama,” alisema Fatma.

Katika hatua nyingine, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema kuwa jeshi hilo halitamuachia Lissu hadi litakapokamilisha upelelezi.

“Bado tunaendelea kumhoji, hatumuachii,” Mkondwa anakaririwa na Mtanzania. “Anatumia kichaka cha ubunge kuchochea uhalifu, tunaye na tukikamilisha upelelezi ni mahakamani,” aliongeza.

 

Wawili wafariki baada ya daladala kugonga treni Dar
Muuguzi kizimbani kwa kumbaka mgonjwa ‘usingizini’