Korea Kusini imesema kuwa imeanza mazungumzo ya moja kwa moja na Korea Kaskazini ili kuutafutia ufumbuzi wa kidiplomasia mgogoro uliopo kwa sasa uliozifanya nchi hizo kuwa katika hali ya sintofahamu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Kang Kyung-wha ambapo amesema kuwa yuko tayari kuanza mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazin iwapo kama fursa hiyo itajitokeza.
”Iwapo kama fursa itapatikana nitafanya mazungumzo naye, kwa sababu ni muhimu sana kujadili hali ya usalama katika nchi zetu, tutajadili namna ya kutatua tofauti zetu ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu,”amesema Kang Kyung.
Aidha, hatua hiyo imekuja mara baada ya Korea Kaskazini kuendelea na mpango wake wa majaribio ya makombora ya masafa marefu, huku ikiendelea na mpango wake wa silaha za nyuklia.
Hata hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura ya kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini dhidi ya mpango wake wa silaha za nyuklia ambazo umekuwa ukipingwa vikali na Marekani.