Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa wapiga kura nchini humo kuondoka kwenye vituo vya kupigia kura na kwenda nyumbani mara baada ya kupiga kura.
Ameyasema hayo wakati akitoa hotuba yake kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la upigaji kura nchini humo, ambapo amesema kuwa ni vyema wananchi wakimaliza kupiga kura warudi majumbani mwao.
“Ombi langu ni kwamba tunapopiga kura, hebu tupige kura kwa amani na tukumbuke kama nilivyosema, kwamba baada ya kupiga kura yako, nenda nyumbani. Nenda kwa jirani yako ukapumzike,” amesema Kenyatta.
Kenyatta amewaasa wananchi wa nchi hiyo kutobaguana ki vyama, kabila, dini kwani Kenya ni nchi yao wote hivyo hakuna haja ya kuchukiana na kubaguana kwa itikadi za kisiasa hasa katika uchaguzi huo.
Kwa upande wake, Muungano wa vyama vya upinzani uliwaasa wapiga kura wao kuto ondoka katika vituo vya kura lakini baadaye ulibadili msimamo huo na kuwataka wakimaliza kupiga kura warudi majumbani mwao.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi nchini humo limesema kuwa limeimarisha ulinzi katika vituo vyote vya kupigia kura hivyo limewaasa wananchi kupiga kura na kurudi majumbani mwao.
.