Meneja wa majogoo wa jiji (Liverpool) Jurgen Klopp, amesisitiza utayari wa kikosi chake katika harakati za kutwaa ubingwa nchini England na kufikia malengo ya kufika mbali kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu wa 2017/18.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani ametangaza msisitizo huo, kufuatia kebehi zinazoendelezwa dhidi yake kutokana na kasi ndogo ya usajili alioonyesha katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
Klopp amesema anaamini wachezaji aliowasajili katika kipindi hiki wanatosha kukiongezea nguvu kikosi chake, ambacho msimu uliopita kilionyesha ushindani wakweli, japo hakikufikia lengo la kumaliza katika nafasi mbili za juu.
“Maneno ya kebehi katika mchezo wa soka ni jambo la kawaida, lakini naamini nina kikosi kizuri ambacho kinaweza kupambana na yoyote msimu huu,” Amesema Klopp.
“Siwezi kumkatisha mtu kauli kwa kusema analolihitaji kuhusu Liverpool, lakini mimi ndio meneja ninajua ninachokifanya katika kipindi hiki ambacho ninakiri ligi ya England na michuano ya Ulaya itakua na ushindani mkubwa kuliko ilivyokua miaka ya nyuma, lakini ninasisitiza nipo tayari kwa mapambano na kushinda.
Baadae leo hii kikosi cha Liverpool kitacheza mchezo wa pili wa ligi kuu ya England dhidi ya Crystal Palace, huku wakikumbuka matokeo ya sare ya mabao matatu kwa matatu waliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza wa ligi hiyo msimu huu dhidi ya Watford.