Aliyekua mlinda mlango wa timu ya taifa ya England Robert Green, amejiunga na klabu ya Huddersfield Town, baada ya kuachwa na klabu ya Leeds United inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini humo.

Green mwenye umri wa miaka 37, ameachwa na klabu ya Leeds United, kufuatia mkataba wake kuvunjwa na uongozi wa klabu hiyo, na sasa ataitumikia Huddersfield kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa mkataba aliousaini.

Green ambaye aliwahi kucheza michezo 650 ya ligi kuu ya England akiwa na klabu za Norwich City, West Ham United na Queens Park Rangers, anatarajiwa kupeleka changamoto miongoni mwa walinda milango wa Huddersfield Town ambayo msimu huu inashirii ligi kuu (PL).

Meneja wa Huddersfield Town David Wagner amesema usajili wa Green umetokana na uzoefu mkubwa alionao kwenye ligi ya England, na anaamini atamsaidia katika michezo muhimu ambayo watacheza katika kipindi hiki cha kusaka mafanikio ya ligi kuu.

“Ninafikiri Rob Green ana kitu cha kipekee, naamini atatusaidia kufanya mambo mazuri kwa kushirikiana na walinda milango wengine klabuni hapa Joel Coleman na Ryan Schofield,” Alisema meneja huyo kutoka nchini Ujerumani.

Huddersfield Town ni mioningoni mwa klabu tatu za ligi kuu ambazo bado hazijapoteza mchezo wowote tangu ligi hiyo ilipoanza, klabu nyingine ambao hazijaonja shubiri ya kufungwa ni Manchester United na Liverpool.

Masau Bwire Aibuka Tena, Asema Bao La Ngoma Halina Utata
ACT Wazalendo kudai mikutano ya hadhara mahakamani