Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte ameliagiza jeshi la polisi kuwaua watu ambao wanakataa/ wanaogoma kukamatwa wakihusishwa na tuhuma za dawa za kulevya, akiwaita ‘wapumbavu’.
Rais Duterte ametoa agizo hilo ikiwa ni siku mbili baada ya kutokea maandamano makubwa ya watu waliotoka kumzika kijana mwenye umri wa miaka 17 aliyeuwa na polisi katika harakati za ukamataji wa watuhumiwa wa dawa za kulevya.
Alitoa tamko hilo muda mfupi kabla hajatoa hotuba rasmi kufuatia mauaji ya Meya wa mji uliopo Kusini mwa nchi hiyo ambayo pia yalihusishwa na watu wanaofanya biashara za dawa za kulevya.
Hata hivyo, aliwataka polisi kuhakikisha kuwa wakati wanafanya ukamataji wanazingatia sheria za nchi na taratibu zote zilizowekwa.
“Nyie kazi yenu ni kuhakikisha mnawazidi nguvu wale wanaokataa kukamatwa,” Rais Duterte aliliambia jeshi la polisi.
“Kama mtu anakataa kukamatwa na anafanya fujo…mko huru kumuua huyo ‘mpumbavu’. Hilo ndilo agizo langu kwenu,” aliongeza.
- Lissu apingwa, atakiwa kutoigeuza TLS kama taasisi yake binafsi
- ‘Handeni’ tatizo la maji bado lakereketa wengi
Imeripotiwa kuwa saa chache baada ya kutoa hotuba yake, alikutana na wazazi wa mtoto mwenye umri wa miaka 17, Kian Loyd delos Santos katika Ikulu ya nchi hiyo.
Rais Duterte alichaguliwa kwa kishindo na wananchi kutokana na ahadi yake ya kuhakikisha kuwa anatumia nguvu ya dola kukomesha biashara ya dawa za kulevya ambayo ilikuwa imeshika kasi nchini humo.
Tangu alipoingia madarakani, mamia ya watuhumiwa wa dawa za kulevya wameripotiwa kuuawa wakipambana na vyombo vya usalama kwa madai kuwa wamepinga kukamatwa.