Mshambuliaji Lionel Messi anaendelea kupambana, kwa kuushawishi uongozi wa klabu ya FC Barcelona ili ufanikishe mpango wa kumsajili rafiki yake kutoka Argentina na klabu ya PSG ya Ufaransa Angel di Maria, kabla ya dirisha la usajili halijafungwa usiku wa kuamkia kesho.
Kwa mara ya kwanza Barca walituma ofa ya Euro milioni 25 kwa ajili ya mshambuliaji huyo lakini ilikataliwa, na baadae wakaongeza hadi kufikia Euro milioni 30.
PSG wameripotiwa kuwa tayari kumuachia mshambuliaji huyo wa pembeni kuondoka katika kipindi hiki, lakini wanashindwa kutoa jibu sahihi kwa viongozi wa FC Barcelona kutokana na kutoridhishwa na ofa zilizowafikia mezani kwao.
Mtandao wa Diario Gol umeeleza kuwa, Messi amekua akizungumza na viongozi wa Barca mara kwa mara ili kusukuma dili hilo likamilishwe kabla ya usiku wa kuamkia kesho.
Messi anatajwa kufanya mazungumzo ya mara kwa mara na Di Maria, kwa lengo la kumshawishi akubali kujiunga na FC Barceona, ili waunde safu imara ya ushambuliaji kwa kushirikiana na Luis Suarez.