Jina la Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe aliyetajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama balozi wake, limelitikisa shirika hilo na kufanya lifikirie upya uamuzi huo.
WHO ilimtangaza Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93 kama balozi wake ikiipongeza Zimbabwe kwa jitihada zake za dhati katika kuimarisha huduma ya afya kwa umma.
Hata hivyo, wakosoaji wa Mugabe walionesha kushangazwa na uteuzi huo wakidai kuwa sekta ya afya nchini humo imezolota na kwamba hata wahudumu wa afya pamoja na madaktari wamekuwa hawalipwi stahiki zao kwa muda.
Ukosoaji mkubwa ulitoka Uingereza na Canada ambazo ni nchi hasimu kisera kwa Rais Mugabe, ambapo wao walienda mbali zaidi katika ukosoaji wao.
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alisema kuwa baada ya kusikia uteuzi huo alidhani ni utani wa ‘siku ya wajinga duniani’ (April fool).
Uingereza ilieleza kuwa uteuzi huo ni wa kushangaza na kwamba unaweza kushusha heshima ya WHO pamoja na Umoja wa Mataifa.
Kutokana na ukosoaji huo ambao umeshika kasi pia kupitia mitandao ya kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom amesema kuwa anafikiria upya pendekezo la kumteua Rais Mugabe kama balozi wa shirika hilo.