Martha O’Donovan’ mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni raia wa Marekani anakabiliwa na tuhuma za kujaribu kuipindua serikali ya Rais Robert Mugabe, Zimbabwe.
Polisi nchini humo wanamtuhumu Martha kuwa ndiye anayendesha ukurasa wa Twitter uitwayo ‘matigary’ ambao uliwekwa maandishi ya kuhujumu na kumkosea heshima Rais Robert Mugabe.
Moja ya maandishi yaliyo kwenye ukurasa huo yameandikwa kuwa ”Nchi yaongozwa na mzee mgonjwa mwenye ubinafsi mkubwa” nukuu.
Martha ambaye anaendesha mtandao wa video za mizaha ya kisiasa amefikishwa mahakamani huko mjini Harare kujibu tuhuma hizo ambapo amekana madai hayo akisema hayana msingi wowote.
Adhabu ya kosa hilo kwa anaepatikana na hatia ni kifungo cha miaka 20 jela.
Kipindi cha miaka michache iliyopita mamia ya watu wamekamatwa nchini humo baada ya kutoa matamshi ya kumsema vibaya Rais Mugabe na kushtakiwa chini ya sheria iliyopitishwa hivi karibuni kuwa kumkosoa Rais ni kitendo cha kihalifu, ambapo Rais Mugabe alimteua waziri atakayeshughulikia usalama na udhibiti wa mitandaoni kuhusu Zimbabwe.