Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameitaka Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wanaboresha mazingira ya masoko yaliyopo kwenye Manispaa hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwenye maeneo hayo bila ya kulazimika kufika katikati ya mji kupata huduma hiyo.
Amesema kuwa wakuu wa idara katika Manispaa hawanabudi kuhakikisha wanashuka kuwafuata wananchi na wafanyabiashara wa masoko hayo na kusikiliza kero zao na kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya masoko hayo ikiwemo majengo, usafi wa mazingira na vyoo.
“Nimeambiwa changamoto nyingi sana na wafanyabiashara wa soko la sabasaba na wamekuwa wakifanya biashara zao kwenye mazingira machafu hali ambayo haizoeleki na haifai kuendelea kuwepo, hivyo manispaa lazima iweke kambi kusikiliza kero zao na kuzitatua, kwani lipo kwenye uwezo wao,” amesisitiza Wangabo.
Aidha, ameitaka manispaa hiyo kuhakikisha usalama wa biashara za wafanyabiashara hao unaimarika ili kupunguza malalamiko yao na kuongeza kuwa atahakikisha malalamiko hayo yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Akielezea changamoto za soko la sabasaba, Mwenyekiti wa soko hilo Feston Mwilema amesema kuwa changamoto kubwa ya soko hilo ni usalama na kuwa hakuna kituo cha polisi na wala hawana mgambo wa kulinda soko hilo, na kuomba kusafisihiwa mazingira kutokana na uchache wa vifaa vya kuzolea uchafu unaozalishwa katika soko hilo.
“Tumelazimika kuchimba shimo la muda la kutupia uchafu unaozalishwa na wauza samaki kutoka na kutokuwepo kwa shimo la kisasa, na tuna kontena moja badala ya matatu ambalo huzidiwa na soko kukosa uzio ni jambo linalotoa mwanya kwa vibaka kuendelea na wizi,” Alisema Mwilema.
Wangabo alitembelea masoko nane yaliyopo kwenye manispaa ya Sumbawanga na kubaini kuwa masoko mengi hayatumiki kwa kukosa miundombinu bora na usimamizi na hatimae wananchi kuanzisha masoko yasiyorasmi na kuhatarisha usalama wa bidhaa zao na usalama wa vyakula kutokana na kuvidandaza chini na kuhatarisha usalama wa wanunuzi.