Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), limesikitishwa kwa hitilafu iliyotokea siku ya mwisho ya usajili usiku wa Desemba 15, mwaka huu kwa kufeli kwa mtandao wa mfumo wa usajili hali iliyosababisha vilabu kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo.
TFF inaendelea na jitihada za kuwasiliana na Mwendeshaji wa mfumo huo waliokasimiwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) walioko Tunis, Tunisia ili kutatua tatizo hilo la kimtandao haraka iwezekanavyo ili kuweza kukamilisha usajili wa dirisha dogo. Katika mawasiliano na kampuni hiyo, FIFA na CAF wamekuwa wakipewa Taarifa ya kila hatua inayochukuliwa na TFF.
Wakati huu ambao jitihada hizo zinaendelea, TFF imevitaka vilabu kuwasilisha nyaraka za usajili wa dirisha dogo katika ofisi za Makao Makuu ya TFF Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
TFF imetoa muda hadi Jumamosi Desemba 23, 2017 kwa vilabu kuwasilisha nyaraka hizo za usajili wa dirisha dogo.
TFF imesisitiza vilabu vyote kuzingatia kusajili kwa wakati pale inapotokea dirisha la usajili limefunguliwa.