Ligi Kuu ya soka Tanzania bara iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inaendelea mwishoni mwa mwezi huu kwa mechi za raundi ya 12 zitakazochezwa kati ya Desemba 29 na 31 mwaka huu, na Januari mosi mwakani.
Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8 kamili mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8 kamili mchana, na saa 4 kamili usiku.
Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).
Hivyo, mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1 kamili usiku.
Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).
Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.
Ligi Daraja la Pili (SDL) itaanza hatua ya pili Desemba 29 kwa Kundi B, C na D wakati mechi za Kundi A zitafanyika kuanzia Desemba 30, 2017.