Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia hatua ya mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Edward Lowassa kumtembelea Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Lissu amejikita katika kauli za Lowassa za kupongeza juhudi na kazi ya Rais Magufuli katika kuleta maendeleo, akidai kauli hizo ni mtaji kwa wapinzani wao.
Mwanasiasa huyo ambaye anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka jana nyumbani kwake mjini Dodoma, alisema sifa hizo pia zitawachanganya wanachama wa chama hicho kutokana na namna ambavyo viongozi wa ngazi za juu wamekuwa wakiikosoa Serikali.
“Vile vile, kauli za aina ambayo tumeisikia leo kutoka kwa Mheshimiwa Lowassa, zina athari kubwa kisiasa. Sio tu zinachanganya wanachama na wafuasi wetu, lakini pia zinawapa mtaji wa kisiasa maadui zetu,” yanasomeka sehemu ya maelezo ya Lissu kwenye akaunti yake ya Instagram.
Ameongeza kuwa kitendo hicho sio cha kunyamaziwa au kuhalalishwa na chama chake kwa ‘hoja nyepesi’.
Lowassa alimtembelea Rais Magufuli jana ambapo kwa mujibu wa Rais, wameshauriana mambo mengi mazuri ambayo hawatayaweka wazi.
Rais Magufuli alimsifu Lowassa kwa kufanya kampeni ya kistaarabu katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kumpongeza pia kwa kazi nzuri aliyoifanya alipokuwa Waziri na Waziri Mkuu wa Serikali zilizopita.