Mapema hii leo uongozi wa klabu ya Simba ulithibitisha taarifa za ujio wa kocha wao mpya Pierre Lechantre ambaye ataanza kazi ya kukinoa kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi mara moja.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa ana sifa lukuki tangu alipokua kicheza soka akiwa nchini kwao Ufaransa, kabla ya kuingia katika tasnia ya ukufunzi wa mchezo huo.
Pierre Lechantre, alizaliwa Aprili 2, mwaka 1950 mjini Lille, Nord, Ufaransa ni kocha aliyeipa Cameroon ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2000 na kabla ya kuanza kufundisha alikuwa mchezani pia.
Aprili 27 mwaka 2012, Lechantre alitambulishwa kuwa kocha Mkuu wa Senegal, lakini akashindwa kufikia makubaliano ya mwisho na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
Akiwa mchezaji katika nafasi ya ushambuliaji, Lechantre amechezea klabu za Paris FC (1986–1989), Red Star 93 (1983–1986), Stade de Reims (1981–1983), Olympique de Marseille (1980–81), RC Lens (1979–80), Stade Lavallois (1976–1979), AS Monaco (1975–76), FC Sochaux (1970–1975) na Lille OSC (1964–1970).
Na akiwa kocha amefundisha timu za taifa za Kongo (2016), Cameroon (1999-2001), klabu za Al-Ittihad Tripoli ya Libya kuanzia 2014 hadi 2015, Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi hadi September 2013, CS Sfaxien ya Tunisia kuanzia Juni hadi Desemba 2010, Club Africain ya Tunisia kuanzia Juni 10 mwaka 2009 hadi Aprili 2010 na Al Rayyan ya Qatar.
Amefundisha pia timu ya taifa ya Mali kuanzia Machi hadi Oktoba 2005, Al-Siliya Sports Club ya Qatar kuanzia Novemba 2003, Al-Ahli ya Jeddah kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2003, Qatar kuanzia Juni 2002, Le Perreux (1992–1995) na Paris FC (1987–1992).
Amewahi pia kuwa Mshauri wa Ufundi wa Val de Marne kuanzia Julai 7 mwaka 1995 hadi Januari 1999.