Chuo Kikuu cha Zimbabwe kimeamua kuweka hadharani utafiti uliofanywa na Grace Mugabe, mke wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe baada ya kuelezwa kuwa idara ya kupambana na rushwa inachunguza uhalali wa shahada ya uzamivu (PhD) aliyotunukiwa na chuo hicho.
Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa uvumi kuwa chuo hicho huenda kilimtunuku kwa upendeleo mama Grace shahada hiyo ya uzamivu mwaka 2014.
Tofauti na wengi walivyotarajia kuwa Chuo Kikuu cha Zimbabwe kingeikabidhi idara hiyo ya kupambana na rushwa kwa ajili ya uchunguzi, chuo hicho kimeamua kuweka kwenye tovuti yake utafiti huo wenye kurasa 226 uliofanywa na Mama Grace ili kila mmoja aweze kuuona na kuthibitisha kuwa alitunukiwa kihalali na sio kwa upendeleo.
Mama Grace alifanya utafiti kuhusu masuala ya familia na malezi ya watoto nchini Zimbabwe, ambapo alieleza kuwa yeye mwenyewe alifanya na kukusanya taarifa.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Zimbabwe, Levi Nyagura hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo ingawa hatua ya kuweka mtandaoni utafiti huo imejieleza.