Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema kuwa Rais Joseph Kabila hatagombea katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Disemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa DRC, Lambert Mende, Rais Kabila amepanga kuachia madaraka muda mfupi baada ya mshindi wa uchaguzi huo kutangazwa na kuapishwa.
Waziri huyo ameiambia Voice of America kuwa mwezi Julai mwaka huu, Rais Kabila anatarajia kumtangaza mtu anayempendekeza kumrithi na ambaye atampigia debe kwenye uchaguzi ujao.
Rais kabila aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya baba yake, Laurent Kabila kuuawa kwa risasi na mlinzi wake ambaye pia aliuawa.
Aligombea urais wa nchi hiyo mara mbili, mwaka 2006 na mwaka 2011 ambapo alishinda katika chaguzi hizo.
Mwaka 2016, Kabila alitakiwa kuwa amekamilisha awamu zake mbili lakini aliahirisha uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kwa madai kuwa mazingira na hali ya kiusalama ya nchi ilikuwa hairuhusu.
Vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia uamuzi huo na kuitisha maandamano mara kadhaa kushinikiza kufanyika kwa uchaguzi haraka iwezekanavyo na Kabila kuachia madaraka.